Pictures : Ze comedy waondoka EATV

17 years ago

  • News
  • KUNDI mahiri la vichekesho la Ze Comedy ambalo lilikuwa likirusha kipindi chake cha ‘Ze Comedy Show’ katika kituo cha Televisheni cha EATV (Channel 5), jana limetangaza kupumzika kwa muda baada ya kuifanya shughuli hiyo kwa takribani miezi minane.
    Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ze Comedy Production, Isaya Mwakilasa ‘Wakuvanga’, akiwa ameambatana na wasanii wenzake wa kundi hilo, alisema kuwa walikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na EATV na baada ya kuifanya kazi hiyo kwa miezi minane na mkataba kumalizika, wameamua kurudi nyumbani na kupumzika kwa muda.
    Mwakilasa alisema, wameamua kurudi nyumbani ili watulie wakiwa huru, huku wakiangalia mtu wa kufanya nao kazi.
    “Tumeamua kupumzika sisi kama sisi, imani yetu ni kuamua kupumzika. Tumekuwa tukifanya kazi pale hadi kufika hapa leo tulipo, tumeamua kurudi nyumbani, kuongeza vionjo na kuwafikia Watanzania wengi zaidi,” alisema Mwakilasa na kuacha mshangao na simanzi kwa watu mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wakiwamo waandishi wa habari.
    Hata hivyo, kiongozi huyo hakuweza kubainisha muda watakaopumzika na watakayefanya naye kazi baada ya mapumziko hayo, zaidi ya kubainisha kuwa tayari wamesajili kundi lao ambalo linajitegemea, linalojulikana kama Ze Comedy Production.
    Kwa upande wake, mtayarishaji (Producer), wa kundi hilo, ambaye awali alikuwa meneja, Sekioni David ‘Seki’, ambaye pia alikuwa mtangazaji wa kipindi cha City Sound kinachorushwa na EATV, alisema kuwa yeye ni chanda na pete na Ze Comedy, na tangu juzi amekuwa katika wakati mgumu kufikia maamuzi ya ama apumzike pamoja nao au awaache na andelee na ajira yake katika kituo hicho.
    “Ni maamuzi ya kijasiri zaidi, mara ya kwanza ilitokea nikiwa Nyota Assemble, ikafikia likagawanyika na kuibuka Nyota Academia, tarehe ya jana (juzi), ulikuwa wakati mgumu, ni maamuzi mazito kuamua kubaki EATV au kuendelea na sanaa kwa sasa hivi. Hivyo kama mnavyofahamu sanaa ndiyo imenifanya nifike hapa nilipo, hivyo nimeamua nibaki na hawa mabwana,” alisema.
    Kuhusu tukio la juzi (Alhamisi), kurudiwa kwa kipindi cha ‘Ze Comedy Show’ ambacho kilishawahi kurushwa siku za nyuma, na je kama hali hiyo itaendelea, Mwakilasa alisema vipindi vyote walivyoviandaa wakiwa EATV ni mali ya kituo hicho na hata jina Ze Comedy Show, na kama wakiamua kuwa wanaendelea kuvirudia hiyo ni hiyari yao.
    Walipoulizwa kuhusu fununu kuwa wanajiunga na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mwakilasa hakukiri wala kukataa, lakini alidai kuwa hivi sasa wameamua kupumzika na wanaweza kuja kufanya kazi na yeyote watakayefikia naye makubaliano.
    Pia alipoulizwa kama wakijiunga na TBC, watakosa fursa huru ya kuonyesha matukio yanayoikosoa serikali na viongozi wake, alidai kuwa hadhani hivyo, kwani chombo hicho kinatokana na kodi za wananchi, hivyo anadhani watakuwa huru kufanya kazi zao kama kawaida bila kufumbwa midomo.
    Mwakilasa aliongeza kuwa, uamuzi huo unawasikitisha kama ambavyo watu wameonyesha kusikitika, lakini pia watakuja kufurahi baada ya mapumziko hayo maana wameamua kujipanga ili kuwafikia Watanzania wengi.
    Lakini habari za uhakika zilizopatikana jana jijini, zinaeleza kuwa kundi hilo linajipanga kuibukia Televisheni ya Taifa, (TBC1).
    Uongozi mpya wa Ze Comedy Production, sasa uko chini ya Mkurugenzi, Mwakilasa, Mkurugenzi msaidizi, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’, Alex Chalamila ‘Mac Regan’ (Ofisa Mipango), Mujuni Silvery ‘Mpoki’ (Ofisa Masoko), Seki (Producer), Lucas Mhuville ‘Joti’ (Mhazini) na Joseph Shamba ‘Vengu’ (Mhazini Msaidizi).
    Awali kabla ya kuanza kuzungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), wasanii hao walifanya ibada fupi ambayo iliongozwa na Masanja.
    Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilimwagia sifa kundi hilo kuwa linafanya kazi kubwa na kuibua na kuikumbusha jamii na serikali katika mambo mbalimbali, hivyo viongozi hawana budi kulikubali badala ya kulichukia.
    0 Comments and 0 replies
arrow_drop_up